PROF. ELISANTE AAGIZA VYAMA VYA MICHEZO NCHINI KUTAMBUA UWEPO NA NGUVU YA BMT

Vyama vya michezo nchini vimeagizwa kutambua na kuheshimu uwepo na nguvu ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kufuata sheria ya Baraza ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya 1971 ili kuhakikisha michezo nchini inasonga mbele.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa kikao na Kamati tendaji ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kilichokuwa na lengo la kufahamiana na kujipanga kwa utekelezaji wa majukumu ya Baraza hasa wakati huu wa serikali ya awamu ya tano yenye kauli mbiu ya hapa kazi tu.

 

 

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akieleza jambo kwa Kamati tendaji ya BMT (hawapo pichani) wakati wa kikao Januari 21,2016.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akieleza jambo kwa Kamati tendaji ya BMT (hawapo pichani) wakati wa kikao Januari 21,2016.

Prof. Ole Gabriel amesema kwamba kama vyama vya michezo Tanzania vitatambua uwepo na nguvu ya Baraza la Michezo la Taifa(BMT) na kulitumia kwa kufuata taratibu na sheria, michezo nchini itaendelea na kuwafanya wanamichezo wetu kutokuwa wasindikizaji na washiriki katika mashindano ya kimataifa bali washindani wenye kuitangaza na kuiletea sifa nchi.

Aliendelea kuwa Wizara haina budi kufanya kazi kwa karibu na Baraza kulingana na sheria ilikuepuka mwingiliano wa majukumu na kuepuka migongano inayopunguza ufanisi wa kazi na maendeleo ya michezo nchini.

Awali kamati ya Utendaji ya BMT ilieleza baadhi ya changamoto zinazolifanya Baraza kukosa meno kuwa ni pamoja na Usajili wa vyama/ Mashirikisho na Vilabu vya Michezo kufanywa na Wizara (IdarayaMichezo) badala ya Baraza la Michezo (BMT) kama ilivyoainishwa kwenye sheria na ukongwe wa Sheria hiyo usiyo kidhi mahitaji ya Michezo kwa sasa.

Changamoto nyingine zilizotajwa ni uduni wa vyanzo vya mapato vya kisheria, Ukosefu wa maadili ya uongozo kwa viongozi wengi wa vyama vya Michezo, Ukosefu wa miundo mbinu ya Michezo na vyuo vya taaluma za Michezo.

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Dioniz Malinzi (shati cheupe) akitoa ufafanuzi wa changamoto zilizopo BMT wakati wa kikao.
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Dioniz Malinzi (shati cheupe) akitoa ufafanuzi wa changamoto zilizopo BMT wakati wa kikao.

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Dioniz Malinzi amewataka viongozi wa vyama vya michezo kutoomba nafasi za uongozi katika vyama kwa ajili ya kujinufaisha bali wazingatie uzalendo katika kukuza na kuendeleza michezo kwa maslahi ya taifa letu.

Malinzi ameiomba serikali kupitia wizara yenye dhamana ya michezo kuhakikisha inahamasisha michezo kwa rika zote kwani michezo ni dawa, afya, kitega uchumi na huleta mahusiano mazuri katika jamii.

Wajumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa ujumla wao wameiomba serikali kuhakikisha kuwa sera na sheria ya Baraza la Michezo la Taifa inafanyiwa maboresho ili iweze kuendana na wakati wa sasa wa sayansi na teknolojia.

Kikao kikiendelea
Kikao kikiendelea

Waliongeza kuwa gharama ya kununua na kuingiza vifaa vya michezo kutoka nje ni kubwa ambapo, waliishauri Serikali kupunguza kodi ya kuingiza vifaa vya michezo na kuongeza shule na vyuo vikuu vya michezo vya Serikali ili kuwa na wataalamu wengi nchini kuepuka kuajiri makocha na wataalam kutoka njena kwa gharama kubwa.

Akijibu hoja za wajumbe katibu Mkuu wa Wizara. Prof. Ole. Gabriel alilitaka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuwa wabunifu na kufikiria namna ya kuanzisha miradi mbalimbali ili kupata fedha za kuijendesha na kuendeleza Michezo, pia aliwataka kuangalia jinsi wanavyoweza kuzungumza na taasisi za Elimu na Ufundi kama vile VETA ili kuanzisha miradi ya kutengeza vifaa vya Michezo kama mipira, Viatu na vinginevyo ili kupunguza gharama za kuagiza vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.

Aliongeza kuwa ni vizuri baraza likawasilisha Wizarani andiko la kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo utakaosaidia kugharamia shughuli mbalimbali za Maendeleo ya Michezo.

Katibu Mkuu huyo aliitaka BMT kuwatafuta na kuwatumia wachezaji wa zamani waliofanya vema katika Michezo mbalimbali kuitangaza nchi na kutumia vyombo vya habari kuhamasisha vijana na wananchi wengi kushiriki katika michezo.

Prof. Elisante alihitimisha kikao hicho kwa kuwaahidi kuyafanyia kazi maombi na maoni ya wajumbe yaliyo ndani ya uwezo wake kwa wakati na yale ya kisheria atafuata utaratibu kuhakikisha yanafanikiwa.

 

 

 

67 total views, 1 views today

Fuatilia Mchezo, like:
0

Leave a Reply

Michezo ni yetu wote, fuatilia, Wataarifu wengi

Follow by Email14
Facebook
Facebook
YouTube0
YouTube
Google+0
Google+
http://nationalsportscouncil.go.tz/blog/2016/01/22/prof-elisante-aagiza-vyama-vya-michezo-nchini-kutambua-uwepo-na-nguvu-ya-bmt/">
RSS