SERIKALI YAWAASA WANAMICHEZO KUTOTUMIA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU KATIKA MICHEZO.
Serikali imewaasa wanamichezo kuacha kutumia dawa za kuongeza nguvu katika michezo.
Rai hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura katika hafla ya kuwaaga na kuwakabidhi bendera wanamichezo wanaokwenda kushiriki na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Olimpiki kwa mwaka huu yanayofanyika Rio dejaneiro nchini Brazil.

Katika hatua nyingine, Serikali imeyashukuru makampuni, mashirika na wadau mbalimbali wa michezo nchini kwa kujitokeza na kuwa mstari wa mbele kushiriki na kudhamini michezo mbalimbali nchini.
Mhe. Anastazia Wambura amesema kuwa wadau wa michezo wamekuwa wakishirikiana na Serikali sio katika suala la michezo pekee hata katika habari na Sanaa na amewapongeza kampuni ya ving’amuzi ya Multichoice Tanzania (DSTV) na Bodi ya Utalii katika azma yao ya kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini.
“Napenda kuwashukuru wadau wetu DSTV na Bodi ya Utalii, nawapongeza kwa kuona fursa hii muhimu na kuitumia katika kuwatia moyo wawakilishi wa nchi yetu katika michezo ya Olimpiki kwa mwaka huu, mueendelee kuiunga mkono Serikali katika kutekeleza sera ya maendeleo ya Michezo ili kufikia malengo yake,” alisema Mhe. Wambura.

Aidha amewataka wawakilishi wa Olimpiki kutumia fursa hii ya wadau wa michezo waliojitokeza kuwaunga mkono ikiwemo DSTV ambao wataonesha mashindano hayo moja kwa moja na kuwafanya watanzania kuwaona, na Bodi ya Utalii kutangaza utalii wa Tanzania kwa mataifa mengine watakayo kutana nayo katika mashindano
ya Olimpiki nchini Brazil.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Bodi ya Utalii waone uwezekano wa kuipeleka timu yetu ya Olimpiki kwenye vivutio vya utalii itakaporejea, na kuwataka BMT kuratibu utaratibu wa timu zetu kuvaa nguo zenye nembo ya wafadhili wetu.
Kwa upande mwingine Prof. Ole Gabriel amewaasa Wanahabari wa michezo kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika habari zenye ukweli na usahihi.
20 total views, 3 views today