KILIMANJARO QUEENS YAIBUKA NA USHINDI WA BAO 3 KWA 0 DHIDI YA BURUNDI

Timu ya Mpira wa miguu ya Wanawake ya Tanzania Kilimanjaro Queens imeibuka kidedea kwa kuifunga bao 3 kwa 0 timu ya Burundi katika shindano lao la kimataifa la kirafiki lililofanyika jana katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

kil2

Mabao yote ya Kilimanjaro Queens yalifungwa kipindi cha kwanza, Bao la kwanza lilifungwa na Asha Rashid dakika ya 22, wakati bao la pili lilifungwa na Mwanahamisi Omary dakika ya 30 huku

Bao la tatu likiwa la kujifunga wao wenyewe baada ya Mabeki wa Burundi kujichanganya na Mchezaji Niyonkulu Saidauze kwenye harakati za kutaka kuokoa mpira kwenye eneo hatari dakika ya 33. Hadi dakika 90 zinamalizika Kilimanjaro Queens ndio walikuwa wababe kwa kutoka na ushindi wa bao 3-0. Mchezo huo wa kirafiki wa Kimataifa uliokuwa ni moja ya Timu zote mbili kujiandaa na Michezo ya CECAFA Nchini Uganda. Na leo Timu zote mbili zinaelekea jijini Jinja, Nchini Uganda.

Michuano ya CECAFA ya kuwania Kombe la Afrika Mashariki na Kati itafanyika kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, 2016 jijini Jinja, Uganda.

kil1

Kwa mujibu wa CECAFA, Tanzania ambayo inaongoza kwa ubora wa viwango vya Mpira wa Miguu kwa nchi za Afrika Mashariki imepangwa kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar pamoja na mwenyeji Uganda.

Tanzania itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12, 2016 kabla ya kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016. Rwanda na Ethiopia zitacheza Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata utepe kwa kucheza na Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na Kenya.

Michezo mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na Kenya zitakazocheza Septemba 13, 2016 ambapo siku hiyohiyo Zanzibar itacheza na Uganda.  Huku Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar wakati  Uganda itafunga hatua ya makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.

Nusu fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika Septemba 20, 2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na nne.

Mashindano ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania inatarajiwa kuanza kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani kwa wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa safari ya Uganda

138 total views, 1 views today

Fuatilia Mchezo, like:
0

Leave a Reply

Michezo ni yetu wote, fuatilia, Wataarifu wengi

Follow by Email14
Facebook
Facebook
YouTube0
YouTube
Google+0
Google+
http://nationalsportscouncil.go.tz/blog/2016/09/09/kilimanjaro-queens-yaibuka-na-ushindi-wa-bao-3-kwa-0-dhidi-ya-burundi/">
RSS