SERIKALI YAAGIZA KUSITISHWA KWA MABADILIKO YANAYOFANYWA NA VILABU VYA YANGA NA SIMBA.

Serikali kupitia Taasisi yake yenye dhamana ya kusimamia michezo nchini BMT imeagiza kusitishwa kwa michakato inayofanyika katika Klabu ya Yanga na Simba.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa Bw. Mohamed Kiganja wakati wa mkutano wake na Waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es salaam.

Kiganja ameeleza kuwa, michakato yote inayoendelea ya kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwa wanachama kwenda kwenye umiliki wa hisa na ukodishwaji kwa vilabu vyote vya michezo usitishwe mara moja hadi hapo marekebisho ya katiba zao kwa mujibu wa sheria ya Baraza la michezo la Taifa na kanuni za msajili namba 442 kanuni ya 11 kifungu kidogo cha (1 hadi 9) yatakapofanyika.

“Baraza linapenda kuona kwamba wahusika wanafuata sheria na taratibu za nchi katika kufikia malengo yao,”alisema Kiganja na kuongeza kuwa:

“Kuendelea na mchakato huu kabla  ya taratibu  za kurekebisha katiba zao kisheria ni kosa na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka maelekezo haya”.

Aliendelea kuwa, hivi karibuni imeibuka michakato ya watu wakitaka kubadilisha umiliki wa vilabu vya wanachama na kuvielekeza kwenye utaratibu wa hisa na ukodishwaji, vitendo hivi vimesababisha migogoro mikubwa ambayo inaashiria uvunjifu wa amani ndani ya tasnia ya Michezo.

“Makundi ya wapenzi na wanachama mamejikita  katika mijadala ambayo hatma yake ni kuzidi kuibomoa jamii badala ya kuijenga na kuimarisha michezo nchini,” alieleza Katibu Mkuu huyo.

Aidha, mpasuko huo umepelekea baadhi ya wanachama wanaoona hawaridhishwi na mwenendo mzima na pengine hata taratibu za suluhu zilizopo kuzikiuka na kuziona hazifai na kuamua kukimbilia mahakamani.

Kiganja alieleza kuwa, athari za kupeleka jambo hili mahakamani ni kubwa kwa vilabu vyetu, Shirikisho la Mpira wa Miguu na Taifa kwa ujumla wake. Kutokana na hali hii, Baraza la Michezo la Taifa kama chombo pekee cha kisheria kilichopewa dhamna ya kusimamia Michezo nchini, hakiwezi kuvumilia ukiukwaji wa Sheria na taratibu unaoendelea ambao unaasharia kutoweka kwa amani kwenye tasnia ya michezo.

Baraza linasitisha michakato yote inayoendelea ya kutaka kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwenye mfumo uliopo sasa,  ni vyema vilabu vikaendelea kubaki kuwa mali ya wanachama,”alisisitiza na kuongeza kuwa:

                                             

Kama kuna mdau yeyote ambaye ana nia ya kumiliki klabu ya mchezo wowote ule ni vyema akaanzisha timu yake kama alivyofanya Bw. Said Salim Bhakhresa kuanzisha klabu ya Azam.

Kwa sasa mijadala ya mabadiliko ndani ya vilabu hivi imefungwa na ni imani ya Serikali kuwa, wale wote waliokuwa wametofautiana kwenye jambo hili watakuwa pamoja kwa maendeleo ya mchezo wa Soka nchini.

 

27 total views, 1 views today

Fuatilia Mchezo, like:
0

Leave a Reply

Michezo ni yetu wote, fuatilia, Wataarifu wengi

Follow by Email14
Facebook
Facebook
YouTube0
YouTube
Google+0
Google+
http://nationalsportscouncil.go.tz/blog/2016/10/26/serikali-yaagiza-kusitishwa-kwa-mabadiliko-yanayofanywa-na-vilabu-vya-yanga-na-simba/">
RSS