IMARISHENI MAHUSIANO NA SERIKALI

01st August, 2017

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka Viongozi wa Shirikisho la ngumi za ridhaa Tanzania kuimarisha mawasiliano na mahusiano na Serikali ili kurahisisha maendeleo ya mchezo huo nchini.

Mhe. Mwakyembe ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi wa Kamati ya Utendaji wa shirikisho hilo ikiwa ni sehemu ya utaratibu aliopanga kukutana na vyama vya Michezo ili kutambua utendaji kazi wao na changamoto zinazowakabili ili Serikali iweze kushirikiana nao kuzitatua.

Hata hivyo amewaahidi Viongozi hao wa  Shirikisho la Masumbwi Tanzania (BFT) kuwatatulia changamoto ya eneo la kufanyia mazoezi pamoja na ofisi ambalo limekuwa likiwakabili kwa muda mrefu pamoja na changamoto nyingine za Shirikisho hilo.

Dkt. Mwakyembe amesema kwamba, kutokana na tatizo la ukosefu wa eneo rasmi la ofisi na sehemu ya kufanyia mafunzo, yeye atawasiliana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi ili kuona namna gani wanaweza kupata eneo kwa ajili ya kulisaidia shirikisho hilo kwa ajili ya kujenga ofisi na eneo la kufanyia mazoezi.

Sambamba na hilo, ameupongeza uongozi wa shirikisho hilo kwa kazi wanazozifanya na kuwataka wazidi kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) hususani katika kupeana taarifa zinazohusu maendeleo ya mchezo wa masumbwi nchini.

“BFT jitahidini muwe na ushirikiano wa karibu na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na msifanye mambo yenu kimya kimya, muwasiliane kwa karibu na BMT kwani hii itasaidia Wizara kushughulikia kero zenu mbalimbali kuliko mkichelewa kutoa taarifa mapema”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Aidha, amewahakikishia kuwa, yupo tayari kutafuta wafadhili ndani na nje ya nchi ili waweze kulisaidia shirikisho hilo kutatua kero za uhaba wa vifaa, rasilimali fedha pamoja na ukosefu wa mafunzo kwa makocha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo amelitaka shirikisho hilo kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Serikali ikiwemo kujenga tabia ya ulipaji kodi, kuwaelimisha Wanamasumbwi kuachana na tabia chafu wanapokuwa michezoni pamoja na kuachana na kujihusisha na madawa ya kulevya.

Kwa upande Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo kwa pamoja wamemuahidi Waziri Mwakyembe na Wizara kwa ujumla kuzingatia masuala mbalimbali ikiwemo kuboresha suala la mawasiliano kati ya Shirikisho na Serikali, kufuatilia suala la mikataba mbalimbali na uwajibikaji wenye kuleta tija kwa Taifa.

 

 

42 total views, 1 views today

Fuatilia Mchezo, like:
0

Leave a Reply

Michezo ni yetu wote, fuatilia, Wataarifu wengi

Follow by Email14
Facebook
Facebook
YouTube0
YouTube
Google+0
Google+
http://nationalsportscouncil.go.tz/blog/2017/08/01/imarisheni-mahusiano-na-serikali/">
RSS