KAMATI YA DKT.MWAKYEMBE YAWEKA WAZI MIKAKATI YA UTEKELEZAJI

Kamati ya ngumi za kulipwa iliyoteuliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe imeeleza mikakati ya utekelezaji wa agizo la Waziri kwa wakati waliopangiwa ili kuhakikisha wanaondoa sintofahamu ya uendeshaji wa ngumi hizo nchini.
Mikakati hiyo imeelezwa leo na Katibu wa kamati hiyo Yahya Poli katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Poli ameeleza kuwa mkakati wao wa kwanza ni kama walivyoelekezwa na Katibu wa Baraza la Michezo Taifa Mohamed Kiganja tarehe 8 Februari alipotangaza kamati hiyo ya Waziri Mwakyembe ambayo ndiyo iliyoteuliwa awali kuandaa Rasimu ya katiba ya ngumi za kulipwa, ikiwa kukusanya maoni kutoka kwa wadau kwa njia ya maandishi na kuongeza kuwa;
“Wadau wanaweza kuwasilisha maoni yao katika Ofisi za BMT zilizopo ghorofa ya pili uwanja wa Taifa au katika tovuti ya baraza www.nationalsportscouncil.go.tz, vilevile mdau anaweza tuma maoni yake kwa njia ya posta sanduku la posta 20116 na kwa barua pepe tpbftz@gmail.com,” alisema Poli.
Aliendelea kuwa, mkakati wa pili wa kamati yake itatangaza tarehe ya kikao cha wadau kujadili rasimu ya Katiba katika kipindi cha siku 12 kutoka tarehe ya leo vile vile ikiwa ni agizo la Waziri.
Aidha, watafanya mkutano na wadau wa ngumi za kulipwa tarehe 20 hadi 23 mwezi huu wakiwemo Makocha/Mameneja, Mawakala/Promota, na wamiliki wa makampuni yanayojihusisha na ngumi za kulipwa Tanzania pamoja na kuwajulisha wadau hao kuhusu kanuni zitakazotumika katika uendeshaji wa ngumi za kulipwa ikiwemo utaratibu wa kupokea na kushughulikia maombi ya kibali cha kusafiri nje ya nchi kushiriki mapambano .
Kamati hiyo ya ngumi za kulipwa inajumuisha wajumbe kumi na tatu ambao ni: Mwenyekiti Emmanuel Saleh, Makamu mwenyekiti Joe Anea, Katibu Yahya Poli na wajumbe ni Habib Kinyogoli, Juma Ndambile, Fike Wilson, Rashid Matumla, Anthony Ruta, Kalama Nyilawila, Jaffari Ndame, Dkt. Killaga Killaga, Shomari Kimbau na Ally C. Bakari.
127 total views, 1 views today