TAGOKA WAAMUA KUENDANA NA SHERIA YA MICHEZO NCHINI

Baadhi ya wanafunzi wa mchezo Karate aina Gojuryu wakiwa katika moja mazoezi ya mchezo huo.
Baadhi ya wanafunzi wa mchezo Karate aina Gojuryu wakiwa katika moja mazoezi ya mchezo huo.

Chama cha Mchezo wa Gojuryu Karate Do – Tanzania (TAGOKA) kupitia baadhi viongozi waliosalia na waliokaa kwa muda mrefu katika uongozi usivyo halali waameamua wafuate Sheria zinazoendesha Michezo nchini kwa kuendelea kufanya mazungumzo na chombo kinachosimamia michezo ambalo ni Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ili kujua njia sahihi ya kufuata ili mchezo na chama chao kiweze kusimama na kuendelea.

Baada ya kufanya mazungumzo na Baraza kwa mara ya kwanza miezi miwili iliyopita, tarehe 10 Januari, 2018 wakiwa zaidi ya Wadau sita kutoka Mikoa tofauti wamefanya tena kikao na BMT kwa mara ya pili kuomba kuhuisha chama chao tena kwa kufuata taratibu zote za msingi wakiomba kuteuliwa viongozi wa muda ili kukiongoza chama kwa muda watakaopangiwa na Baraza na kufanya watakayoelekezwa ili kukipeleka chama na mchezo panapostahili kisheria.

Aidha, Mmoja wa viongozi waliosalia katika chama hicho ambacho hakifanyi majukumu yoyote ya mchezo huo, ambaye aliteuliwa kama Makamu Mwenyekiti Heri Kivuli ameeleza kuwa, hawakuwa wanafuata taratibu za kisheria  kuendesha chama hicho kwakuwa hata katiba ilitengenezwa na mtu mmoja kwa kunakili katiba ya nchi nyingine, pamoja na viongozi kuteuana tu bila uchaguzi.

“Kwa kweli tumekaa muda mrefu tangu uongozi wetu ulipoingia madarakani na hatukuwa tunachaguana bali kupendekezana tu na Katiba iliyokuwa ikitumika ilinakiliwa na kiongozi mmoja kutoka katiba ya mchezo huo kutoka nchi nyingine bila kujali hali halisi ya nchi yetu, sasahivi nimejifunza mengi baada viongozi wa BMT kutueleza na naamini hili tunalofanya likifanikiwa tutafika mbali,” alieleza Kivuli.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kikao hicho Afisa Maendeleo ya Michezo wa Baraza ambaye anasimamia chama hicho  Milinde Mahona aliwaeleza wadau hao wa mchezo wa Karate aina ya Gojuryu kuwa, ameyachukua maelezo yao na atayafikisha kwa Mtendaji  Mkuu wa BMT na watapata majibu mapema ili kuendelea na hatua nyingine za maendeleo ya mchezo huo.

Mahona aliendelea kuwa, pindi tu majibu yatakapotolewa wajiandae kutekeleza mambo muhimu ya kwanza kwa maendeleo ya chama na mchezo ikiwemo marekebisho ya katiba pamoja na usajili wake, kuhakikisha vilabu vimesajiliwa, kuandaa uchaguzi mkuu, kuhamasisha wanachama wapya, kuwa na Ofisi, akaunti ya kuweka pesa za chama na kuwa na mipango mikakati ya maendeleo ya chama na mchezo huo ikiwemo kalenda ya matukio ya mwaka 2019.

Aidha, katika kikao hicho wadau hao walipendekeza majina ya viongozi wa muda iwapo Mtendaji wa Baraza ataona inafaa ili waweze kutekeleza majukumu ya chama kabla ya uchaguzi mkuu akiwemo, Mwenyekiti Heri – Kivuli, Makamu wake – Philiph Chikoko, Katibu Mkuu – Fahari Doruta, Katibu Msaidizi – Paul Mkumbwa, Mweka hazina – Suleiman Al-adawi na wajumbe ni Flowin Madiwa, Yusuph Kimvuli, Mohamed Zubeir na Ally Unji.

 

 

Fuatilia Mchezo, like:
0

Leave a Reply

Michezo ni yetu wote, fuatilia, Wataarifu wengi

Follow by EmailO
Facebook
Facebook
YouTube0
YouTube
Google+0
Google+
http://nationalsportscouncil.go.tz/blog/2019/01/10/tagoka-waamua-kuendana-na-sheria-ya-michezo-nchini/">
RSS